SOMO..Yak 2:1-9 Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu. Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu, je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu? Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao? Bali ninyi mmemvunjia heshima maskini. Je! Matajiri hawawaonei ninyi na kuwavuta mbele ya viti vya hukumu? Hawalitukani jina lile zuri mliloitwa? Lakini mkiitimiza ile sheria ya kifalme kama ilivyoandikwa, Mpende jirani yako kama nafsi yako, mwatenda vema. Bali mkiwapendelea watu, mwafanya dhambi na kuhukumiwa na sheria kuwa wakosaji.

Wimbo wa Katikati
Zab 34:1-6
Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.
(K) Maskini huyu aliita, Bwana akasikia

Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana akanijibu,
Akaniponya na hofu zangu zote.
(K) Maskini huyu aliita, Bwana akasikia

Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote.
(K) Maskini huyu aliita, Bwana akasikia

Somo la Injili
Mk 8:27-33
Siku ile Yesu alitoka na wanafunzi wake, wakaenda kwenye vijiji vya Kaisaria-Filipi; na njiani akawauliza wanafunzi wake, akasema, Watu huninena mimi kuwa ni nani? Wakamjibu, Yohana Mbatizaji; wengine, Eliya; wengine, Mmojawapo wa manabii. Naye akawauliza, Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani? Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo. Akawaonya wasimwambie mtu habari zake. Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka. Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi. Petro akamchukua, akaanza kumkemea. Akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro, akasema, Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.

Neno la Bwana…sifa kwako ee Kristo

*ASALI MUBASHARA-Alhamisi 20/02/2020*

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika Zaburi ya wimbo wa katikati linasisitizia juu ya upendo alio nao mwenyezi Mungu kwa maskini. Kwa hakika Bwana huwasikiliza maskini, mbele yake maskini wanayo hadhi kuu. Mbele ya Bwana maskini akilia haonekani kuwa kama msumbufu bali husikilizwa katika huruma kuu.

Tabia hii ya kimungu ni tafauti na tabia inayooneshwa na baadhi ya wakristo wa enzi za Yakobo na Yakobo anakemea udhaifu wa namna hii. Wakristo wake walionekana kuwastahi zaidi matajiri kuliko maskini, cha ajabu kabisa ni kwamba tabia hii iliingia hadi kanisani, kwamba tajiri alionekana kuwa mkristo bora zaidi na wa maana kuliko maskini. Tajiri alipoingia kanisani, alionekana kama roho mtakatifu ameingia ndani ya kanisa. Hivyo baadhi ya waaamini walianza kumpatia heshima zaidi. Yakobo anakemea tabia za namna hii-kwanza kwa sababu humfanya Mungu atambulike kama Mungu mbaguzi, mwenye kuwapenda matajiri na kuwachukia maskini, pili, huwafanya wakristo watoe heshima zaidi kwa mwanadamu zaidi kuliko Mungu kwani kila alipo tajiri au kiongozi mkubwa, heshima huelekezwa zaidi kwake na hii humfanya Mungu asiabudiwe katika kina.

Neno hili litufundishe na sisi pia. Tusiwe na ubaguzi maishani mwetu hasa makanisani mwetu. Kanisani ni mahali ambapo wote wanapaswa kusikilizwa, hasa maskini na wagonjwa. Faraja yao ipo kanisani. Kanisa liwapatie faraja hii.

Kanisa liliundwa kwa nguvu na uwezo ya Roho Mtakatifu na sio kwa nguvu ya fedha. Wakristo wengi wa mwanzo waliohusika katika kueneza injili wengi walikuwa maskini na wagonjwa. Matajiri walikuwa wachache. Hata ikiwa kanisa litakosa matajiri au likikosa majengo mazuri au wasomi wakubwa-bado litazidi kuwepo na kuwa na nguvu kwani Roho ndiye afanyaye kazi ndani ya kanisa. Tuepuke kuwastahi matajiri zaidi kuliko maskini.

Katika somo la injili, Bwana Yesu anawauliza wanafunzi wake juu ya utambuzi wake yeye mwenyewe, kwamba watu hunena kwamba yeye ni nani? Petro anatoa jibu zuri, na Yesu anafurahishwa na jibu hilo na pia anaendelea mbele kumwelezea Petro juu ya utume na wajibu unaoambatana na cheo chake cha umasiha kwamba itambidi ateswe na kuuawa kabla ya kufufuka.

Petro hakubaliani na mtazamo huu na hivyo anataka kumpinga Yesu na Yesu anatumia maneno makali kabisa kumpinga Petro, anamwita Petro kuwa shetani, na hivyo akae nyuma. Yesu alifanya jambo zuri, la kutafuta utambulisho wake toka kwa wanafunzi wake na alifurahi kupata utambulisho wake toka kwa wanafunzi wake.

Sisi nasi tunapaswa kuuliza juu ya utambulisho wetu katika eneo tunaloishi-hii itatusaidia katika kujielewa zaidi. Wapo kati yetu ambao hatujielewi na pia maisha yetu hayaeleweki. Tukishirikiana na wenzetu, tutaweza kujitambua zaidi na kuwa watu bora zaidi.

Hivyo siku ya leo, mwulize mwenzako, je, mimi ni nani hapa? Maisha yangu yakoje hapa? Ninatimiza wajibu wangu vipi? Majibu yao yaweza kuwa msaada mkubwa sana kwetu. Pia tusisite kuwakemea tena kwa ukali wale wanaotutaka tubadili mwenendo na msimamo wetu bora. Yesu alimkemea Petro kwa ukali. Nasi tuwakemee marafiki wabaya, na wote walio na mawazo potofu yawezayo kuharibu maisha yetu.

:copyright:Pd. Prosper Kessy OFMCap.

*NB: SHAJARA ZA 2020 ZA ASALI MUBASHARA -Zenye tafakari ya kina zipo zakutosha wasiliana nami 0755444471 au 0714002466. Jipatie shajara hii ikufundishe namna ya kuchambua masomo na jinsi ya kujisogeza karibu na Mungu kwa njia ya Neno lake, “Kutokufahamu maandiko nikutokumfahamu Kristo”-Mt.Jerome.