ASALI MUBASHARA-Jumanne 18/02/2020

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo neno la Bwana katika asubuhi ya leo tutaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na fundisho juu ya faida za majaribu. Yakobo anakubali kwamba majaribu yapo, lakini atakayeweza kukabiliana nayo hadi mwisho huyo hukubalika kwa Mungu na hujipatia tuzo kuu. Mtu wa namna hii ni yule awezaye kuona faida iliyopo katika vishawishi, yaani kuiimarisha Imani ya mwanadamu. Na hili kweli ni jambo ambalo maishani tunakumbana nalo. Ukikutana na mtu ambaye majaribu kama magonjwa yamekuja kwake na kwa njia ya yale majaribu ameikweza ile imani yake-kwa kweli huyu huwa ni wa pekee. Huyu huwa siku zote ni imara katika imani, hayumbishwi na vitu vidogo vidogo ndani ya imani yake. Huyu kweli huwa na Imani. Ni kama shahidi aliyeepukika kifo. Lakini ukikutana na yule ambaye hajawahi kukutana na majaribu yoyote, kwa kweli imani yake mara nyingi huwa ni dhaifu na huwezi kujua kwamba kweli huyu mtu ana imani au anafuata mkumbo. Halafu kuna wale wengine ambao majaribu yamekuja na kuwafanya wapoteze Imani, wanabadilika kabisa. Walipokuwa bila majaribu, walikuwa wanakuja kanisani kila siku lakini baada ya majaribu, hata kanisani hawafiki. Mtu wa namna hii huwezi kusema kwamba alikuwa na imani kubwa kwa Mungu. Mungu ameruhusu majaribu kutaka imani yake na mtazamo wake wa imani ubadilike, uimarike lakini kwa sababu yeye alikuwa na vionjo vyake na mategemeo yake kama Yakobo anavyotueleza katika somo la kwanza, basi akaishia kupoteza.

Ndugu zangu, Imani yetu lazima iimarishwe na majaribu-na majaribu yanapokuja, mtakatifu yakobo anasema lazima tuyakubali kwani aliyekwisha pokea majaribu huyo anayo imani bora kuliko yule ambaye hajawahi kuona jaribu lolote. Hivyo yabidi kufurahia majaribu.

Na hili suala la majaribu tunakutana nalo tena katika injili. Tutasikia katika injili wanafunzi wa Yesu wakiogopa kwa sababu hawakuchukua mikate. Wanajiuliza kwamba je, tutakula nini? Mbona itakuwa njaa tu huku? Wanajilaumu. Lakini Yesu anasikitika. Anaona kwamba kumbe hawa watu wake hawana imani. Yaani wamekwisha niona nikitenda miujiza mingi na kumbe ile miujiza walikuwa hata hawaitilii maanani? Kumbe walikuwa hawaoni kana kwamba nalikuwa natenda miujiza? Hivyo, Yesu anasikitika kwa sababu wanachukulia vitu kimzaha mzaha mno. Anaona kwamba matendo yake yote anayowafanyia hayawajengi kiimani. Hivyo, Watu KAMA HAWA WANGEHITAJI MAJARIBU YA MMOJA MMOJA ILI WAMTAMBUE YESU KUWA NI NANI. ILE MIUJIZA YA PAMOJA INAWAFANYA WENGINE WASHINDWE KUMSHUHUDIA AU KUMTAMBUA YESU KWA SABABU LABDA ANAPOKUWA ANAITENDA WENGINE UNAKUTA WAKO BUSY NA MAMBO YAO NA NDIO MAANA HAWAWEZI KUJIFUNZA TOKA KWA HIYO MIUJIZA. HIVYO, WALIHITAJI JABIBU MOJA MOJA LIWAFUNZE.

Hivyo ndugu zangu leo tunaalikwa kuangalia majaribu yote ambayo tumewahi kukutana nayo maishani. Yaangalie, ona kama yamewahi kukuimaraisha. Kama yameshindwa kukuimaraisha lazima ubadilike. Hapa ni kukosa imani kama hawa mitume wa leo. Usikubali ugonjwa, au jaribu lolote likufanye uwe sababu ya wewe kushindwa kiimani. Tusimtukane Mungu, Yakobo anatuambia kwamba Imani yetu ikiimarishwa kwa njia ya majaribu, basi tutastahili tuzo kubwa. Maneno haya yatutie moyo kuvumilia majaribu yetu.

©Pd. Prosper Kessy OFMCap.

NB: SHAJARA ZA 2020 ZA ASALI MUBASHARA -Zenye tafakari ya kina zipo zakutosha wasiliana nami 0755444471 au 0714002466. Jipatie shajara hii ikufundishe namna ya kuchambua masomo na jinsi ya kujisogeza karibu na Mungu kwa njia ya Neno lake, “Kutokufahamu maandiko nikutokumfahamu Kristo”-Mt.Jerome.