“MBEGU ZA UZIMA”
Tafakari ya kila Jumapili
Jumapili, Februari 16, 2020.
Dominika ya 6 ya Mwaka A wa Kanisa

YbS 15:16-21;
Zab 118:1-2, 4-5, 17-18, 33-34;
1Kor 2:6-10;
Mt 5:17-37

KUSHIKA SHERIA!

Mungu anatuita sio katika maisha ya maadili tu, lakini katika hali ya kuishi ya juu zaidi. Tunatembea kuelekea ukamilifu kwa kujitahidi daima kuchagua kufanya mazuri. Katika hali ya asili sisi sio wakamilifu, lakini Mungu anatuita tutafakari jinsi tunavyo ishi na kutambua ni kipi kimeenda vibaya na kipi kimeenda vizuri. Kwa kutafakari maisha yetu kwa kupitia njia ya Imani maisha yetu yanakuwa katika hekima. Yesu anatufundisha dini ambayo itatufanya ikuwa ndani yetu na kuwa sehemu ya maisha yetu.

Somo la kwanza linatualika tufanye kila jitihada ya kufanya uchaguzi sahihi katika maisha. Yoshua bin Sira anatangaza kwamba amri za Mungu zina nguvu ya kuokoa. Musa aliwaambia watu alivyokuwa karibu na mto Yordani kwamba anawapa nafasi yakuamua: maisha na mafanikio, kifo na maangamizi. Uchaguzi ulikuwa wao kuamua. Yoshua bin Sira sasa anawaambia watu, akisisitiza ujumbe ule wa Musa kwamba Mungu ameweka mbele yao moto na maji, maisha na kifo, mema na mabaya. Wanatusukuma nasi tufanye uchaguzi sahihi kwa kusema kwamba macho ya Mungu huwaelekea wale wenye kutenda mema. Ni ujumbe mzito kwetu kwamba hatuwezi kufuta mawazo yetu na matendo yetu kutoka kwa Mungu.

Injili ya Mathayo kwa asili iliandikwa kwa ajili ya Wayahudi Wakristu, inaweza kuonekana kama maneno ya kufariji kwao. Mathayo daima amekuwa akirejea Agano la Kale kuwaonesha kuwa maisha ya Yesu hajaja kuvunja sheria za zamani za Wayahudi bali ni mwendelezo wa yote ambayo yalitabiriwa na manabii hapo zamani. Maisha na mafundisho ya Yesu hayapaswi kuonekana kama ni dini mpya, maisha ya Yesu ni maisha ya asili ya habari ya Ukombozi. Anawahakikishia wasomaji wake kwamba Yesu hakuja kutengua Sheria bali amekuja kuikamilisha. Kwa hiyo, sheria bado ina nafasi yake na hivyo haitatupwa mbali hadi pale itakapo timiza jukumu lake. Kwasababu kwa Yesu, maana halisi ya sheria inaweza kufupishwa kwa neno moja “heshima”. Heshima kwa Mungu, kwa jina lake, kwa siku yake, heshima kwa wazazi, heshima kwa uhai, utu, heshima kwa ukweli na heshima kwa jina la mtu na hatimaye heshima kwa nafsi. Kwa maneno mengine sheria yote inahitimishwa kwa ‘heshima kwa Mungu’ na ‘heshima kwa nafsi” na jirani. Kwasababu heshima hii haijalimbikizwa katika visheria vidogo na miiko bali imejibeba katika amri ya mapendo: Upendo kwa Mungu na upendo kwa jirani. Yesu hakutambulisha sheria mpya bali alitambulisha njia mpya yakufikiria na kuelewa sheria. Hakutengua sheria wala kubadili bali alienda mbele zaidi ya kile kinacho hitaji. Kwasababu kwa Yesu, hali ya nje tu ya kushika sheria haitoshi. Kuwa mfuasi wa Yesu ni vizuri kutambua sheria iliojengwa katika mapendo. Kushika sheria bila mapendo ni sawa na kuwa na mwili bila roho. Ndio maana anawaambia wafuasi wake kwamba fadhila zao zisipo zidi zile za Mafarisayo na Waandishi, hawataingia katika Ufalme wa Mungu.

Ili kuwafanya wafuasi wake waelewe mafundisho yake, Yesu aliwapa mifano sita mizito na katika injili ya leo tuna minne, tuna kuhusu: hasira, uasherati, talaka na kiapo. Anasema wazi kwamba haitoshi tu kushika ambacho sheria inatuambia bila kutenda fadhila zinazo ambatana nazo. Kwa Yesu, hakuwezi kuwa na utengano kati ya uhusiano wetu na Mungu na watu. Mkristo anapaswa kumpata Mungu kwa watu wote na katika uumbaji.

Sala: Bwana, nifanye niwe safi moyoni. Nifanye niweze kuwa mtu mwaminifu na mwenye kujali utu. Ninaomba ukweli ulio uweka ndani ya moyo wangu uweze kuwa msingi wa matendo yangu na maneno yangu. Ninaomba niongee nikiwa na dhamiri safi kila wakati nikiongea ulichonipa niongee. Yesu, nakumini wewe. Amina.