MASOMO YA MISA, FEBRUARI 14, 2020
IJUMAA YA WIKI YA 5 YA MWAKA

SOMO 1
1Fal. 11:29-32; 12:19

Ikawa zamani zile Yeroboamu alipokuwa akitoka katika Yeroboamu alipokuwa akitoka katika Yerusalemu, nabii Ahiya, Mshiloni, alikutana naye njiani; naye Ahiya amevaa vazi jipya, na hao wawili walikuwa peke yao mashambani. Ahiya akalishika lile vazi jipya alilokuwa amelivaa, akalirarua vipande kumi na viwili. Akamwmbia Yeroboamu, Twaa wewe vipande kumi, maana Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nitaurarua ufalme, na kuuondoa katika mkono wa Sulemani, nami nitakupa wewe kabila kumi; lakini yeye atakuwa na kabila moja kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya Yerusalemu, mji ule niliouchagua katika miji yote ya kabila za Israeli. Hivyo Israeli wakaasi juu ya nyumba ya Daudi hata leo.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 81:9-14 (K) 10, 8

(K) Mimi ndimi Bwana Mungu wako: Isikieni sauti yangu.

Usiwe na mungu mgeni ndani yako
Wala usimsujudie mungu mwingine.
Mimi ndimi Bwana Mungu wako
Niliyekupandisha toka nchi ya Misri. (K)

Watu wangu hawakuisikiliza sauti yangu,
Wala Israeli hawakunitaka.
Nikawaacha wakaenda kwa ukaidi wa mioyo yao,
Waenende katika mashauri yao. (K)

Laiti watu wangu wangenisikiliza,
Na Israeli angeenenda katika njia zangu;
Ningewadhili adui zao kwa upesi,
Na juu ya watesi wao ningegeuza mkono wangu. (K)

SHANGILIO
Mdo. 16:14

Aleluya, aleluya,
Ee Bwana ufungue moyo wetu, ili tuyatunze maneno ya Mwanao.
Aleluya.

INJILI
Mk. 7:31 – 37

Yesu alitoka katika mipaka ya Tiro, akapita katikati ya Sidoni, akaenda mpaka bahari ya Galilaya, kati ya mipaka ya Dekapoli. Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono. Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi, akataama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri. Akawaonya wasimwambie mtu; lakini kadiri ya alivyozidi kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari; wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.