MASOMO YA MISA, FEBRUARI 13, 2020
ALHAMISI YA WIKI YA 5 YA MWAKA

SOMO 1
1Fal. 11:4-13

Mfalme Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake. Kwa kuwa Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni, na Milkomu, chukizo la Waamoni. Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, wala hakumfuata Bwana kw autimilifu, kama Daudi baba yake. Sulemani akamjengea Kemoshi, chukizo la Wamoabi, mahali pa juu, katika mlima uliokabili Yerusalemu, na Moleki, chukizo la wana wa Amoni. Na kadhalika ndivyo alivyowafanyia wake zake wa nchi za kigeni, waliofukiza uvumba, wakawatolea miungu yao dhabihu.Basi Bwana akamghadhibikia Sulemani kwa sababu moyo wake umegeuka, naye amemwacha Bwana, Mungu wa Israeli, aliyemtokea mara mbili, akamwamuru Bwana. Kwa hiyo Bwana akamwambia Sulemani, Kwa kuwa umefanya hayo, wala hukuyashika maagano yangu, na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme usiwe wako, nami nitampa mtumishi wako. Walakini katika siku zako sitafanya haya, kwa ajili ya Daudi baba yako; nitaurarua utoke katika mkono wa mwana wako. Lakini sitaondoa ufalme wote pia; nitampa mwana wako kabila moja, kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, na kwa ajili ya Yerusalemu niliouchagua.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 106:3-4, 35-37, 40 (K) 4

(K) Ee Bwana utukumbuke, kwa kibali uliyonayo kwa watu wako.

Heri washikao hukumu,
Na kutenda haki siku zote.
Ee Bwana, unikumbuke mimi,
Kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako,
Unijilie kwa wokovu wako. (K)

Walijichanganya na mataifa,
Wakajifunza matendo yao.
Wakazitumikia sanamu zao,
Nazo zikawa mtego kwao. (K)

Naam walitoa wana wao nab inti zaoKuwa dhabihu kwa mashetani.
Hasira ya Bwana ikawa juu ya watu wake,
Akauchukia urithi wake. (K)

SHANGILIO
Yak. 1:21

Aleluya, aleluya,
Kwa upole lipokeeni neno lile lilipandwa ndani, linaloweza kuziokoa roho zenu.
Aleluya.

INJILI
Mk. 7:24 – 30

Yesu aliondoka Nazareti akaenda zake hata mipaka ya Tiro na Sidoni. Akaingia katika nyumba, akataka isijulikane na mtu; lakini hakuweza kusitirika. Ili mara mwanamke, ambaye binti yake yuna pepo mchafu, alisikia habari zake, akaja akamwangukia miguuni pake. Na yule mwanamke ni Myunani, kabila yake ni Msirofoinike. Akamwomba amtoe pepo katika binti yake. Akamwambia, Waache watoto washibe kwanza; maana si vizuri kukitwaa chakula cha watoto, na kuwatupia mbwa. Naye akajibu, akamwambia, Naam, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto. Akamwambia, Kwa sababu ya neno hilo, enenda zako; pepo amemtoka binti yako. Akaenda zake nyumbani kwake, akamkuta yule kijana amelazwa kitandani, na yule pepo amekwisha kumtoka.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.