ASALI MUBASHARA-Ijumaa 14/02/2020

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika asubuhi ya leo kwenye somo la kwanza, tunakutana na habari za kugawanyika kwa ufalme wa Israeli. Kugawanyika huku kulisababishwa na kosa la mfalme Solomoni, kiburi chake na kutokumjali Mwenyezi Mungu na kuamua kama alivyoongozwa na marafiki zake.

Mwishowe anailetea famila ya Daudi maanguko makubwa. Anaifanya ipoteze uongozi wa makabila kumi ya Israeli. Hakika Solomoni ni mfalme mwenye historia yenye kujaa mambo ya ajabu. Alikuwa mfalme mwenye hekima kuliko wote katika familia ya Daudi lakini pia alikuwa mfalme aliyeleta hasara kubwa sana kwa familia ya Daudi. Leo ufalme juu ya makabila 10 anapewa Jeroboam.

Hakika tunalo kubwa la kujifunza toka kwa Solomoni. Hakika shetani hupendelea watu maarufu, wale wenye ushawishi, wale wenye vyeo vyao. Kadiri unavyokuwa maarufu, ndivyo na shetani anavyokuja karibu yako kwa lengo la kukuangusha akijua kwamba endapo atafanikiwa kumwangusha mtu maarufu, basi ataweza kueneza uovu wake kwa walio wengi zaidi. Hivyo tuwe watu wa kujichunga zaidi na zaidi. Kila tujionapo kuwa na cheo au umaarufu, ndivyo shetani anavyotaka kutuangusha.

Kila unapojitahidi kukaribia utakatifu, ndivyo shetani naye anavyojitahidi kukuleta chini. Tutambue mbinu hizi na tuombe tusije tukaanguka kama ilivyokuwa kwa Solomoni. Wapo tuliokabidhiwa mamlaka ya kiroho na kiserikali kuhusu wenzetu, tuombe ili tusije tukawa sababu ya wenzetu kuanguka zaidi kwani shetani hupenda kuwatumia walio maarufu zaidi ili kusababisha madhara makubwa kwa wengi.

Kila mwenye madaraka ajichunguze kila siku ili asije kuwa sababu ya kutumika kama mjumbe wa shetani.

Katika somo la injili Bwana Yesu anamponya Bubu na kiziwi. Anawezesha ulimi wake kusema na masikio yake kusikia. Huyu aliyekuwa Bubu na kiziwi kwa hakika alipitwa na mengi. Udhaifu wake wa kuwa Bubu na kiziwi ulimfanya mara nyingi ashindwe kutambua kinachoendelea kwenye jamii yake, pia kulimfanya ashindwe kujua njia na namna za kujihami yeye mwenyewe.

Sisi siku ya leo tuombe kufunguliwa kuhusu ukiziwi wetu na ububu wetu. Sisi ni viziwi wa sheria na maongozi ya Mungu. Ni viziwi pia wa kutoa heshima kwa viongozi wetu. Pia ni bubu wa kuongea matendo makuu ya Mungu na mazuri kuhusu wenzetu. Mara nyingi midomo yetu imependelea kuongea machafu na mabaya kuhusu wenzetu. Tumwombe Mungu tuweze kufunguliwa midomo yetu ipate kuongea mazuri kuhusu wenzetu. Tumsifu Yesu Kristo. Na leo tunapofanya kumbukumbu ya wapendanao, tumshukuru Mungu kwa uwepo wa wote wenye kutupenda. Lakini akiwapo anayekuchukia, basi, tumwachie Mungu.

©Pd. Prosper Kessy OFMCap.

NB: SHAJARA ZA 2020 ZA ASALI MUBASHARA -Zenye tafakari ya kina zipo zakutosha wasiliana nami 0755444471 au 0714002466. Jipatie shajara hii ikufundishe namna ya kuchambua masomo na jinsi ya kujisogeza karibu na Mungu kwa njia ya Neno lake, “Kutokufahamu maandiko nikutokumfahamu Kristo”-Mt.Jerome.