ASALI MUBASHARA-Alhamisi 13/02/2020

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza tunakutana na habari za kuanguka kwa Solomon. Solomoni aliyekuwa na hekima nyingi, aliyesifika akiwa mfalme kijana aliyeweza kutambua yaliyo muhimu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu, aliyeweza kuwavutia wafalme toka mbali hadi Israeli na kuifanya Israeli ijulikane duniani kote, siku ya leo anakosa hekima yote na kuadhibiwa. Hakika ni jambo la kusikitisha, hadi tunajiuliza, nini kilichotokea kwa Solomoni?

Kilichomwangusha Solomoni hakikutoka mbali. Ni vile vitu alivyojivunia navyo na kumpatia umaarufu, hekima yake na marafiki wake. Kwanza, hekima yake ilifika mahali ikamletea kiburi, akajiona kujua kila kitu, akaona kwamba anafanana na Mungu. Ukosefu wa unyenyekevu ukawa mwanzo wake wa kuanguka. Pili, wale marafiki waliovutiwa kwake kutokana na ile hekima, wale marafiki hasa waliokuwa na jinsia tofauti walikuja kumbadilisha na kumfanya ageukie dhambi zaidi. Mwishowe Solomoni anaanguka vibaya.

Siku ya leo tujifunze kutambua hatari iliyopo katika yule tunayemwita rafiki. Tumchunguze tupate kutambua ni wapi huyu rafiki anatupeleka. Tujiulize, je, huyu rafiki ananifanya niwe na kiburi au unyenyekevu? Je, tangu nianze kumfahamu, nimemheshimu Mungu zaidi?

Pia tujiulize kuhusu vipaji vyetu, au kazi zetu tufanyazo, je, hizi zimetuletea unyenyekevu zaidi? au ndio zimetufanya tuwe na kiburi cha kupindukia kila siku? Tusiache kumcha Mungu. Mungu ndiye umaarufu wote. Unyenyekevu utatupatia mambo yote.

Kwenye somo la injili, Bwana Yesu anakutana na mama asiye Myahudi anayekuja kuomba msaada wa kuponywa toka kwa Yesu. Yesu anamjibu mama huyu kwa ukali wakati anatoa ombi lake kwa sababu mama huyu alikuwa mama wa imani ya kipagani na hivyo angaliweza kutendewa miujiza na mwishowe kushindwa kutofautisha ule muujiza na ushirikina.

Hivyo Yesu alimjibu kwa ukali ili kuimarisha imani yake, ili imani yake itambue kwamba muujiza wa Yesu ni kwa anaye amini. Mama huyu anakuwa mnyenyekevu na hakika unyenyekevu wake unamfanya aponywe.

Sisi tutambue kwamba katika kuomba, tuwe na unyenyekevu kama wa huyu mama. Twaweza kukutana na watu wenye lugha chafu, wakati wa kuomba wanakusumanga sana lakini tujifunze kuvumilia pale tunapoomba.

©Pd. Prosper Kessy OFMCap.

NB: SHAJARA ZA 2020 ZA ASALI MUBASHARA -Zenye tafakari ya kina zipo zakutosha wasiliana nami 0755444471 au 0714002466. Jipatie shajara hii ikufundishe namna ya kuchambua masomo na jinsi ya kujisogeza karibu na Mungu kwa njia ya Neno lake, “Kutokufahamu maandiko nikutokumfahamu Kristo”-Mt.Jerome.