WAKATI mchakato wa kuelekea kumtangaza Mwalimu Julius Nyerere kuwa Mtakatifu ukiendelea katika hatua za awali, kwa baadhi ya Watanzania wamekuwa hawafahamu kuwa kuna michakato miwili ya Watanzania wenzetu kuelekea kuwa Watakatifu kwa Imani Katoliki, nao ni mwalimu Julius Nyerere na Sista Bernadeta Mbawala wa huko Peramiho, Songea Mkoani Ruvuma.

 

Kwa mwalimu Nyerere aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania wengi wanamfahamu kwa namna mbalimbali. Swali, Je vipi kwa Sista Bernadeta Mbawala?

 

Jibu lake lipo. Punde muumini mkatoliki anapokuwa mtakatifu jina lake linatumika kama mfano bora kwa waumini wengine wa dhahebu hilo na pengine jina lake hutumiwa katika maombi mbalimbali na ata picha zake kuwekwa sehemu za ibada. Kuweza kujua namna ya maisha yalivyokuwa pindi alipokuwa hai basi Kanisa katoliki hufanya mchakato wenye hatua kadhaa hadi kumtangaza muumini huyo kuwa mtakatifu.

Hatua hizo ndizo wanazopitia sasa Julius Nyerere na Sista Bernadeta Mbawala. Kusudio kubwa la mchakato huo ni kuwafanya waumini wa kanisa hilo kuiga maisha mema aliyoishi mtakatifu fulani. Msomaji wa makala haya sina haja ya kukuuliza kama unamfahamu Julius Nyerere lakini sina budi kukuuliza juu ya Sista Bernadeta Mbawala.

 

Maisha yake kwa ujumla yalikuwa ya kipekee mno na pengine ni ngumu kuhakiki nani hasa alikuwa wa kwanza kubaini karama za mtawa huyu lakini kwa sababu inawezakuwa masista wenziwe, lakini hawakuweka kumbukumbu hizo, na kama hawakutoa taarifa ni vigumu kuthibitisha hilo, lakini taarifa rasmi na ambazo ni sahihi, mtu wa kwanza kugundua alikuwa ni Baba yake mshauri wa Kiroho padre mmoja Mswisi ambaye aliweza kuandika matini ndogo juu ya maisha ya Sista Bernadeta.

 

Hilo linatoa taswira moja kubwa ya kuhifadhi kumbukumbu zetu ziwe za masuala ya dini na mengineyo kwa faida ya vizazi vijavyo. Ndani ya kumbukumbu zilizohifadhiwa tunaweza kugundua mengi na kujifunza mengi punde panapoonekana pana karama fulani.

“Ee baba wa mbinguni, kwa njia ya mtumishi wako Sista Benadeta Mbawala, umelipatia kanisa lako, katika ulimwengu huu uliojaa mateso na magonjwa, ushuhuda mkubwa, juu ya nguvu za ukombozi zipatikanazo kwa msalaba wako mtakatifu. Kwa maombezi ya mtumishi wako, utujalie kwa wema wako usio na kipimo, tupate yale tunayoomba (TAJA OMBI LAKO).Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristu Bwana wetu. Amina.” Hii ni sala inayoonekana katika kijarida maalumu kilichotolewa na jimbo Katoliki la Songea baada ya mchakato huo wa kuelekea kutangazwa mtakatifu kuanza mwaka 2011.

 

“Nafahamu Sista Bernadeta ni mtumishi wa Mungu nimekuwa nikimuomba mara nyingine na kufanikiwa, naomba kupitia kwake, muniombee kwani mahusiano na mkuu wangu wa kazi si mazuri hata wafanyakazi wenzangu hawanisemeshi, naomba Mungu aingilie kati kupitia maombezi yake. Pia mke wangu amekuwa mgonjwa kwa miaka mingi akisumbuliwa na UKIMWI baada ya kuanza novena ya Sista Bernadeta mwezi huu ameongezeka uzito toka kilo 50 hadi 55 na hajaugua malaria na hata uso wake unang’aa watu wanashangaa.” Haya yamesemwa na muumini mmoja wa kanisa hilo lakini kwa mujibu wa mwongozi wa kumtangaza mtu kuwa mtakatifu miujiza hiyo inapelekwa Vatikani na huko kamati maalumu ya uchunguzi itachunguza na kama mambo yakienda vizuri mtu huyo hutangazwa mtakatifu.

“Jambo hili la miujiza lazima lihakikishwe na wizara inahusika na masuala haya linaweza kumuita  mhusika na kumuhoji kama alitumia dawa yoyote au kweli amepona kwa miujiza na jambo hilo likihakikiswa ndipo suala hilo linaweza kwenda hatua nyengine.”Anasema Padre Titus Amigu wa Jimbo Katoliki la Lindi.

 

Kama alivyosema Padri Amigu na wakati hayo yakiendelea, waamini wengine wakienda katika eneo lililokuwa kaburi la mtawa huyu na kuchukua udongo ambao inaaminika kuwa wakipata miujiza kwa udongo kutoka kaburini humo.

 

Jambo hili lilitia shime kwa Jimbo Katoliki la Songea kuanzisha mchakato huo mwaka 2011kama nilivyokudokeza mara baada ya kupata kibali kutoka Vatikani. Kazi ilianza na ilipofika Januari 24, 2012 masalia ya Sista Bernadeta Mbawala yalichimbuliwa kaburini mwake.

 

Jambo hili ambalo ni geni nchni Tanzania lilifanyika mbele ya maaskofu wa metropolitani ya Songea ambayo inahusisha majimbo nane Katoliki ambayo ni Songea, Njombe, Mbinga, Mbeya, Iringa,Tunduru-Masasi,Lindi na Mtwara. Huku watu wengi wakivutika kuona kilichomo ndani ya kaburi baada ya maziko ya miaka 50.

“Mwanzoni tulidhani hakutakuwa na kitu baada ya kukuta mchwa wengi lakini tulipochimba zaidi tlishangaa kuiona mifupa yake, punje za rozari na msalaba” Anasema Padri Francis Shawa ambaye yuko kwenye kamati ya mchakato huu.

Kwa sasa masalia hayo yamehifadhiwa katika kikanisa cha Askofu Mkuu Mwashamu Norbert Mtega wa jimbo kuu Katoliki la Songea. Baadaye kuhifadhiwa katika Kanisa Kuu la Kiaskofu Songea.

 

Sista Bernadeta Mbawala alizaliwa Oktoba 27, 1919 Miaka 100 iliyopita katika kijiji cha Likuyufusi jirani na Peramiho. Wazazi wake wakiwa ni Stephen Msikazonge na Agatha Mayanda. Mtawa huyu alijiunga na Jumuiya ya masista Wabenidiktine ya sista wa sista Agatha Chipole na huku alionekana kuwa na karama kubwa za kiroho katika mambo mbalimbali wakati wa uhai wake.

 

Maisha yake ya utawa alijaliwa na Mungu kuweza kuishi kwa muda mfupi mpaka pale kifo kilipomchukua Novemba 29, 1950 kutokana na ugonjwa wa kifua Kikuu.

 

Wazazi wake kama nilivyokudokeza Stefani na Agata walikuwa ni miongoni mwa Wakristu wa kwanza Peramiho. Katika ubatizo alipewa jina la Klara. Alipokuwa mtoto aliingia shule ya misheni ya Peramiho na alipotimiza umri wa miaka 18 aliingia utawa akaitwa Sista Bernadeta. Akaweka nadhiri zake za kwanza Novemba 11, 1934.Sista Bernadeta alikuwa mgonjwa kwa muda wa miaka 17 na baadaye alifariki dunia.

Mwisho.

Adeladius Makwega

Ketaketa–Morogoro.