ASALI MUBASHARA-Jumatatu 20/01/2020

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika Zaburi ya wimbo wa katikati linaelezea juu ya faida ya utii kwa sheria ya Mungu. Mungu anafurahishwa na yeyote mwenye kuipendelea sheria yake. Sadaka inayotoka kwa mtu mtiifu kwa sheria za Mungu, hata kama ni ndogo kiasi gani, humpendezesha Mungu.

Mfalme Sauli katika somo la kwanza ameshindwa kuonesha utiifu kwa sheria ya Mungu. Alikubali furaha ya mafanikio ya vita imtawale na kuanza kuzifurahia nyara, kinyume cha maagizo aliyoyapokea toka kwa Mwenyezi Mungu. Na wakati Sauli akigawanya nyara, akichukua mali alizopora toka kwa Waamaleki, moyo wake ulikuwa na majivuno na kumsahau Mungu. Japokuwa Sauli alijitahidi kuchukua baadhi ya nyara alizopora katika vita na kumtolea Mwenyezi Mungu sadaka, Mwenyezi Mungu hakufurahishwa na sadaka hii kwani ilitoka katika moyo wenye kujaa majivuno na kiburi na uliokuwa umemsahau Mwenyezi Mungu.

Sisi tusiige mfano wa Sauli. Upo wakati Mwenyezi Mungu atatuletea mafanikio maishani mwetu. Yafaa tuwe makini na kutumia kipindi hiki vyema kwani tukikitumia vibaya, twaweza kuanguka sana. Mungu hutoa mafanikio akiwa na lengo la kutupima kuangalia jinsi tutakavyokuwa watii. Wapo baadhi yetu tumenyanganywa hata kile tulichopewa kidogo na Mwenyezi Mungu baada ya kuonesha majivuno baada ya kupewa. Kila tupatapo mafanikio, tukumbuke shetani yupo karibu na hivyo tutunze mafanikio hayo kwa njia ya sala.
Tuepuke kuruhusu furaha ya mafanikio itufanye tumsahau Mungu.

Katika somo la injili, anasisitiza kwamba divai mpya iwekwe kwenye viriba vipya. Kamwe usiweke divai mpya kwa viriba vibovu kwani viriba hivyo vitapasuka. Ujumbe huu toka kwa Yesu utufundishe kuelewa kwamba mambo matakatifu hayapaswi kuchanganywa na maovu. Tujifunze kuyapatia mambo matakatifu nafasi njema naya pekee maishani mwetu. Kama tunataka kweli kuwa watu wema na wachamungu, lazima tufanye kila kitu kipya. Kama ni mazingira, lazima tuyabadili. Tuanze na mazingira mapya, kama ni marafiki, tuanze na wapya.

©Pd. Prosper Kessy OFMCap.