SOMO 1 .. Kulikuwa na mtu mmoja wa Benyamini, jina lake akiitwa Kishi, mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia, mwana wa Mbenyamini, mtu shujaa, mwenye nguvu. Naye alikuwa na mwana, aliyeitwa jina lake Sauli, kijana, tena mzuri; wala katika wana wa Israeli hakuwako mtu mzuri kuliko yeye; tangu mabega yake kwenda juu alikuwa mrefu kuliko watu wote.

Na punda za Kishi, baba yake Sauli, walikuwa wamepotea. Kisha akamwambia Sauli mwanawe, Haya basi, twaa mtumishi mmoja pamoja nawe, uondoke, uende ukawatafute punda hao. Naye akapita kati ya nchi ya milima milima ya Efraimu, akapita na kati ya nchi ya Shalisha, lakini hawakuwaona; kisha wakapita kati aya nchi ya Shaalimu, wala huko hawakuwako; wakapita kati ya nchi ya Wabenyamini, lakini hawakuwapata.
Hata Samweli alipomwona Sauli, Bwana akamwambia, Huyu ndiye niliyekuambia habari zake; huyu ndiye atakayewamiliki watu wangu. Ndipo Sauli akamkaribia Samweli langoni, akasema, Tafadhali uniambie, nyumba ya mwonaji iko wapi? Samweli akamjibu Sauli, akasema, Mimi ndimi mwonaji; tangulia mbele yangu ukwee mpaka mahali pa juu, kwa maana mtakula pamoja nami leo; kisha, asubuhi nitakuacha uende zako, nami nitakuambia yote uliyo nayo moyoni mwako.

Ndipo Samweli akatwaa kichupa cha mafuta, akayamimina kichwani pake, akambusu, akasema, Je! Bwana hakukutia mafuta uwe mkuu juu ya watu wake Israeli? Nawe utamiliki watu wa Bwana, na kuwaokoa na mikono ya adui zao; kisha hii itakuwa ishara kwako ya kuwa Bwana amekutia mafuta uwe mkuu juu ya urithi wake.Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu. (1 Sam. 9:1-4, 17-19; 10:1)

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 21:1-6 (K)

(K) Ee Bwana, mfalme atazifurahia nguvu zako.

Ee Bwana, mfalme atazifurahia nguvu zako,
Na wokovu wako ataufanyia shangwe nyingi sana.
Umempa haja ya moyo wake,
Wala hukumzuilia matakwa ya midomo yake. (K)

Maana umesogezea Baraka za heri,
Umemvika taji ya dhahabu safi kichwani pake.
Alikuomba uhai, ukampa,
Mda mrefu wa siku nyingi, milele na milele. (K)

Utukufu wake ni mkuu kwa wokovu wako,
Heshima na adhama waweka juu yake.
Maana umemfanya kuwa Baraka za milele,
Wamfurahisha kwa furaha ya uso wako. (K)

SHANGILIO
Lk. 4:18-19

Aleluya, aleluya,
Bwana amenituma kuwahubiri maskini habari njema, kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao.
Aleluya.

INJILI
Mk. 2:13-17

Yesu alitoka, akaenda kando ya bahari, mkutano wote ukamwendea, akawafundisha. Hata alipokuwa akipita, akamwona Lawi wa Alfayo, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate. Akaondoka akamfuata.
Hata alipokuwa ameketi chakulani nyumbani mwake, watoza ushuru wengi wa wenye dahmbi waliketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake; kwamaana walikuwa wengi wakimfuata. Na waandishi na Mafarisayo walipomwona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Yesu aliposikia aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi; sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

*ASALI MUBASHARA- Jumamosi 18/01/2020*

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi hii. Leo katika neno la Bwana tunamsikia Yesu akisema kwamba amekuja kwa wagonjwa na si kwa wenye afya; hawa ndio wadhambi kama akina Matayo mtoza ushuru, makahaba kama akina Maria Magdalena na yule mwizi aliyetubu akiwa msalabani. Cha kushangaza ni kwamba wale wagonjwa wanafurahi na kumpokea Yesu kwa furaha na ndio wanaourithi ufalme wa Mungu. Wanaojiona sio wagonjwa wao ndio wanaompinga Yesu; hawa ndio Wafarisayo na mwishowe tutasikia kwamba watajifungia hata ufalme wa mbingu.

Hapa tuna la kujifunza ndugu zangu, tunapokuja kwa Mungu, lazima tujione kuwa wadogo, wanyenyekevu. Hawa ndio wanaofaulu mbele ya Mungu. Lakini wanaokuja mbele ya Mungu wakijiona kwamba ni wafalme, nakwambia huwa hawafiki mahali na wote huishia hivihivi tu. Unapofika mbele ya Mungu, fika na udhaifu wako, fika na ujinga wako, fika na makosa yako. Usifiche makosa yako yote na kuanza kuonesha ukuu wako, ukubwa wako, majitoleo yako, jinsi utoavyo sadaka kama yule Mfarisayo alivyofanya mbele ya mtoza ushuru. Wewe hakikisha huachi udhaifu wowote, yeye anamwilika ndani ya roho zote na anatufahamu vizuri zaidi.

Hiki ndicho kitakachokusaidia kusimama mbele ya Kristo na kumpatia Kristo arekebishe udhaifu wetu. Mfalme Sauli tunayemsikia katika somo la kwanza japokuwa alikuwa na uzuri wake, alichokosa kama tutakavyoendelea kusoma huko mbeleni ni ile roho ya kujishusha, kuja kwa Mungu na udhaifu wake. Hiki ndicho alichokosa. Alikuwa anakwenda na makuu yake tu na hivyo alishindwa kumpatia Mungu nafasi arekebishe hayo mapungufu yake.

Hivyo, tunapokuja kusali leo, tusisahau kuja na mapungufu yetu. Yaoneshe mbele ya Mungu na hivyo utafanikiwa kumpatia Mungu nafasi. Usiwe kama yule mfarisayo aliyejikuja mbele ya Mungu na CV safi na kusahau ni dhaifu mbele ya Mungu. Twende mbele ya Mungu kama tulivyo nakufungua moyo wote na kumwambia wewe Bwana wanijua nilivyo dhaifu naomba unipe afya ya roho yangu na mwili pia.

:copyright: Pd. Prosper Kessy OFMCap.