SOMO 1 1Yon. 4:11-18 Wapenzi, ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote. Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, nap endo lake limekamilika ndani yetu. Katika hili tunafahamu ya kuwa tunakaa ndani yake, naye ndani yetu, kwa kuwa ametushirikisha Roho wake. Na sisi tumeona na kushuhudia ya kuwa Baba amemtuma Mwana kuwa Mwokozi wa ulimwengu. Kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu.

 

Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake. Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu; kwa kuwa, kama yeye alivyo, ndivyo tulivyo na sisi ulimwenguni humu. Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lilio kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 72:1-2,10,12-13 (K) 11

(K) Mataifa yote ya ulimwengu, watakusujudia, ee Bwana.

Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako.
Na mwana wa mfalme haki yako.
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu. (K)

Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi,
Na wingi wa Amani hata mwezi utakapokoma
Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
Toka mto hata miisho ya dunia. (K)

Wafalme wa Tarshisi na visiwa walete kodi,
Wafalme wa Sheba na Seba na watoe vipawa.
Naam, wafalme wote na wamsujudie;
Na mataifa yote wamtumikie. (K)

Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,
Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi
Atamhurumia aliye dhaifu na maskini,
Na nafsi za wahitaji ataziokoa. (K)

SHANGILIO
Lk. 4:18-19

Aleluya, aleluya,
Bwana amenituma kuwahubiri maskini habari njema, na kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao.
Aleluya.

INJILI
Mk. 6:45-52

Baada ya watu elfu tano kula na kushiba, mara Yesu aliwalazimisha wanafunzi wake wapande mashuani, watangulie kwenda ng’ambo hata Bethsaidia, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Hata alipokwisha kuagana nao akaenda zake mlimani kuomba.
Na kulipokuwa jioni mashua ilikuwa katikati ya bahari, na yeye yupo peke yake katika nchi kavu. Akawaona wakitaabika kwa kuvuta makasia, kwa maana upepo ulikuwa wa mbisho; hata ilipopata kama zamu ya nne ya usiku akawaendea, akitembea juu ya bahari; akataka kuwapita. Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe, kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni mimi, msiogope. Akapanda mle chomboni walimo; upepo ukakoma; wakashangaa sana mioyoni mwao; kwa maana hawakufahamu habari za ile mikate, lakini mioy yao ilikuwa mizito.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

*ASALI MUBASHARA-Jumatano 08/01/2020*

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la injili, tunapata kutafakari habari za wanafunzi wa Yesu wakiwa katika hofu kubwa, upepo unawasumbua, unawatesa, wanatumia nguvu zao wakipambana nao bila mafanikio.

Baadaye Yesu anajitokeza katikati yao na wanapomuona wanaongezeka tena katika hofu badala ya kupata matumaini. Wanapiga yowe tena wakifikiri kwamba Yesu ni mzima au pepo mchafu amewavamia. Hofu na wasiwasi waliokuwa nao umewafanya washindwe kumtambua Yesu wakati wa matatizo yao na kumfananisha na mzimu. Ndivyo inavyotokea na kwetu kila siku. Wengi wetu tuna hofu na wasiwasi, hivi ni vitu vibaya sana. Vimetufanya tukose iman na kufanya maamuzi ya ajabu.

Wanafunzi walipokuwa katika hofu wamefanya maamuzi ya ajabu. Sisi tuogope kufanya maamuzi hasa wakati tunapokuwa na hofu na wasiwasi mkubwa. Yafaa kwenda mbele ya Mungu kila ujisikiapo hofu kwani maamuzi yoyote utakayofanya katika hofu na wasiwasi ni maamuzi yaliyokosa imani. Unapokuwa katika hofu, habari inayozunguka kichwani yaweza kuwa ni kuhusu pepo wabaya na watu wenye roho mbaya wakitaka kukudhuru. Kila kitakachotokea utakiona kwa macho ya pekee. Ukiona mjusi chumbani utamwita pepo mchafu, muda wote utatembea katika wasiwasi. Hata chumbani utashindwa kulala peke yako. Tujifunze kupambana na hofu zetu.

Katika somo la kwanza, Yohane anasisitiza kwamba kupendana, na anaeleza kwamba katika pendo hakuna hofu, hakuna kumdhania mwenzako vibaya. Somo hili linatuhimize juu ya hatari ya hofu. Tukitaka kuishi na wenzatu katika pendo, tuepuke kumdhania vibaya na hofu za kila siku. Zipo methali zisemazo kikulacho ki nguoni mwako lakini yafaa kwa hakika kuzichunguza methali za namna hii kabla ya kupokea mafundisho yake. Zaweza kutufanya tushindwe kuishi vyema na wenzetu.

:copyright:Pd. Prosper Kessy OFMCap.