MASOMO YA MISA, JANUARI 4, 2020

SOMO 1
1Yoh. 3:7-10

Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki kama yeye alivyo na haki; atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu.
Katika hili watoto wa Mungu ni Dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu yeyote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 98:1, 7-9 (K) 36

(K) Miisho yote ya dunia, imeuona Wokovu wa Mungu wetu.

Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. (K)

Bahari na ivume na vyote viijazavyo,
Ulimwengu nao wanaokaa ndani yake.
Mito na ipige makofi,
Milima na iimbe pamoja kwa furaha,
Mbele za Bwana,
Kwa maana anakuja aihukumu nchi. (K)

Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa adili. (K)

SHANGILIO
Yn. 1:14,12

Aleluya, aleluya,
Naye neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu.
Aleluya.

INJILI
Yn. 1:35-42

Siku ile, Yohana alikuwa amesimama pamoja na wawili katika wanafunzi wake. Akamtazama Yesu akitembea, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu! Wale wanafunzi wawili wakamsikia akinena, wakamfuata Yesu. Yesu aligeuka, akawaona wakimfuata, akawaambia, Mnatafuta nini? Wakamwambia, Rabi, (maana yake, Mwalimu), unakaa wapi? Akawaambia, Njoni, nanyi mtaona. Wakaenda, wakaona akaapo, wakakaa kwake siku ile. Nayo ilikuwa yapata saa kumi.
Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliomsikia Yohane na kumfuata Yesu. Huyo akamwona kwanza Simoni, ndugu yake mwenyewe, akamwambia, Tumemwona Masihi (maana yake, Kristo). Akampeleka kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama, akasema, Wewe u Simoni, mwana wa Yohane; nawe utaitwa Kefa (tafsiri yake Petro, au Jiwe).

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.