Ndugu zangu karibuni kwa adhimisho la misa Takatifu. Kikuu tunachopata katika masomo yetu ni kwamba, Kumfuata Yesu ni kuwa Kiumbe Kipya: Katika injili ya leo, wanafunzi wa Yohane Mbatizaji wanamwacha Yohane Mbatizaji na kumfuata Yesu. Wanamfuata kwa sababu sasa wameelewa juu ya ukuu wa Yesu; kwamba yeye ndiye mwenye kuyashika matumaini ya dunia na vyote vimewekwa chini yake (Kol 1:17). Hivyo wanafunzi wa Yohane wana kila sababu ya kuambatana na Yesu.

Nasi sote tunaalikwa kumfuata huyu Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu. Katika somo la kwanza, Yohane anatukumbusha kwamba tunapomfuata Yesu, lazima tuchukie uovu na tuwe watenda haki na tuache maisha yetu ya zamani. Lazima kuwa kiumbe kipya. (Ndiyo maana hata Simoni anapokuja kwa Yesu katika injili ya leo jina lake linabadilika na kuwa Petro kuonyesha kwamba utu wake wa kale umepita). Tusikubali kubakia watu wale wale wakati tukimpokea Yesu anatufanya upya. Basi, tusivumilie kuona dhuluma na uonevu ukitendeka mbele ya macho yetu kwani Kristo hakuvumilia dhuluma na uonevu.Tuepuke kuwa mashaidi wa uongo.

Tumuombe Yesu tukisema, Ee Yesu nisadie niwe mfuasi wako. Nipatie jina jipya na utambulisho mpya nipate kuwa mfuasi wako kweli.

©Pd. Prosper Kessy OFMCap