MWADHAMA Kadinali Polycarp Pengo, Jumapili ya leo ameongoza ibada ya misa katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mwokozi Sinza jijini Dar na kusisitiza kuwa amani ya kweli inatoka kwa Mungu kupitia mwanaye Yesu Kristo.

Katika mahubiri yake, Kadinali Pengo alianza kwa kuelezea historia ya uumbaji kwa kueleza jinsi ambavyo ulimwengu ulikuwa na mtafaruku kabla Mungu kuleta amani ya kweli duniani.

“Tukisoma katika kitabu cha Mwanzo, tunaona jinsi ambavyo Mungu mwenyewe aliileta amani duniani. Aliumba vitu mbalimbali kisha kumuumba mwanadamu na kumuweka katika bustani nzuri aitawale lakini baadaye shetani aliingia na kuleta mtafaruku,” alisema Kadinali Pengo.

Katika Injili, Baba Kadinali Pengo alizungumzia pia jinsi ambavyo Mungu aliamua kumleta mwanaye wa pekee Yesu Kristo katika njia ya ubinadamu baada ya kuona watu wamemuasi Mungu na kuishi katika mafarakano.
“Amani ya kweli inapatikana kupitia Bwana wetu Yesu Kristo, tunaweza kujiona tuna amani katika mambo mengine lakini kwa kweli tunajidanganya.

Amani ya kweli inapatikana kupitia Yesu. Huyu Yesu ambaye tunaazimisha ufufuko wake leo ndio mfalme wa amani, tuyaishi maisha yake na mwisho wa siku tuuendee utakatifu,” alisema Kadinali Pengo.

Baada ya kumalizika kwa ibada ya misa hiyo, Paroko Cuthbert Maganga (SDS) alimshukuru Kadinali Pengo kwa kushiriki ibada hiyo ya Krismasi pamoja na waumini wa Sinza ambao walikuwa wamemmisi kwa muda mrefu.
“Kwa kweli baba Sinza tulikumisi sana. Tunasema asante kwa kutuongozea ibada ya Misa Takatifu leo na kutulisha chakula cha kiroho, asante sana baba na Mungu akubariki,” alisema Padri Maganga.

 

Pia alimueleza kuwa, kwa mapendo makubwa, vyama mbalimbali vya kitume vikiwemo Uwaka, Wawata, Viwawa na Wazee na Wastaafu vimetoa matoleo maalum kama zawadi ya Krismasi.

Na Erick Evarist