Juma la 3 la majilio
Mtakatifu Ammon, shahidi
Ijumaa 20 Desemba 2019
Somo la 1
Isa. 7:10 – 14

Siku zile, Bwana alisema na Ahazi akinena, Jitakie ishara ya Bwana, Mungu wako; itake katika mahali palipo chini sana, au katika mahali palipo juu sana. Lakini Ahazi akasema, Sitaitaka, wala sitamjaribu Bwana. Naye akasema, Sikilizeni sasa, enyi nyumba ya Daudi; Je! Ni neno dogo kwenu kuwachosha wanadamu, hata mkataka kumchosha Mungu wangu pia? Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.

Wimbo wa katikati
Zab. 24:1–6

Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.
(K) Mfalme wa utukufu apate kuingia.

Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe.
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili.
(K) Mfalme wa utukufu apate kuingia.

Atapokea Baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo.
(K) Mfalme wa utukufu apate kuingia.

Shangilio

Aleluya, aleluya,
Ee ufunguo wa Daudi, ufunguaye milango ya ufalme wa milele, njoo kuwaokoa watu wako waliofungwa katika gereza la giza.
Aleluya.

Injili
Lk. 1:26–38

Malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu.
Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema. Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani?
Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepta neem akwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.
Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.
Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.