ASALI MUBASHARA-Jumamosi 21/12/2019

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu katika adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi mada yetu kuu tunayojifunza ni kwamba Yesu ni sababu ya furaha; ujio wake ni furaha. Mama Maria anayembeba Yesu alipofika kwa Elisabeth, Elisabethi alifurahi kabisa, matatizo yake yaliyokuwa yakimwandama kwa kuwa na mimba aliyasahau na kushangilia. Na hata kitoto kilichokuwa ndani ya tumbo lake kilishangilia kwa furaha.

Somo la kwanza linatumia pichaa ya mpendwa anayetembea juu ya milima akija kutangaza furaha. Huyu mpendwa ni Yesu na leo inadhihirika jinsi anavyokuwa sababu ya Elisabethi kufurahi. Kama alikuwa sababu ya Elisabethi kufurahi, hakika atakuwa sababu yetu kufurahi pia, hakika tukimuamini hatatuacha katika hali ya kukosa imani na kukata tamaa na matumaini.

Hakika Yesu anapaswa kuwa sababu ya sisi kufurahi, tunapaswa kuangalia ni kipi kinachotufanya Yesu asipate kuwa sababu ya sisi kufurahi na kubakia katika huzuni. Kikubwa ni tamaa, kutokuridhika na kile nilichonacho na kutojiamini na kile nilichopewa na Bwana.

Kutoridhika na kile tulichopewa na Bwana kimetufanya tuwe watu wa kuwaangalia wengine tu, tukitamani vya kwao na kusahau kukuza kipaji tulichopewa na Bwana na ndio sababu wengi wetu ni maskini. Basi tusikubali Yesu apite kwetu kila siku na sisi kushindwa kupata furaha kama Elisabethi-lazima tujiulize ni kitu gani hicho kinanizuia?

Maria alimpeleka Yesu kwa Elisabethi na hapa Elisabethi alipata kufurahi. Sisi tujifunze kuwapelekea wenzetu Yesu, yaani habari njema. Hata kama tunaoujumbe wa kuonya au kukaripia wenzetu, lazima tujifunze namna ya kuwaeleza ili basi nao wafarijike, mara nyingi tumetumia lugha au mazingira mabaya na ndio maana tumeishia kuwaletea wenzetu machungu makubwa.

Sisi tuwe kama Maria, tukifika kwa wenzetu wafurahi. Pia kipindi hiki tuwakumbuke pia mayatima, tuwapelekee Yesu, tuwachangie kitu, ni namna ya kuwaeleza kwamba Kristo ni wetu sote; basi tufurahi.

© Pd. Prosper Kessy OFMCap.