MASOMO YA MISA, DISEMBA 17, 2019
JUMANNE, JUMA LA 3 LA MAJILIO

SOMO 1
MWA. 49:2, 8 – 10

SIKU ILE, Yakobo aliwaita wanawe, akawaambia: Kusanyikeni, msikie, enyi wana wa Yakobo, msikilizeni Israeli, baba yenu.
Yuda, ndugu zako watakusifu, mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako. Wana wa baba yako watakuinamia. Yuda ni mwanasimba, kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda; aliinama akajilaza kama simba, na kama simba, na kama simba mke; ni nani atakayemwamsha? Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, wala mfanya sharia kati ya miguu yake, hata atakapokuja yeye, mwenye milki, ambaye mataifa watamtii.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 72:1 – 4, 7 – 8, 17 (K) 7

(K) Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.

Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako,
Na mwana wa mfalme haki yako.
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu. (K)

Milima itawazalia watu Amani,
Na vilima navyo kwa haki.
Atawahukumu walioonewa wa watu,
Atawaokoa wahitaji, atamseta mwenye kuonea. (K)

Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi,
Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.
Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
Toka Mto hata miisho ya dunia. (K)

Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,
Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi.
Atamhurumia aliye dhaifu na maskini,
Na nafsi za wahitaji ataziokoa. (K)

Jina lake na lidumu milele,
Pindi ling’aapo jua jina lake liwe na wazao;
Mataifa yote na wajibariki katika yeye,

SHANGILIO
Aleluya, aleluya,
Ee Hekima ya Aliye juu, unayepanga yote kwa nguvu zako na utaratibu mwema, uje kutufunza njia ya busara.
Aleluya.

INJILI
Mt. 1:1 – 17

Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu.
Ibrahimu akamzaa Yuda na ndugu zake; Yuda akamzaa Peresi na zera kwa Tamari; Peresi akamzaa Esromu; Esromu akamzaa Aramu; Aramu akamzaa Aminadabu; Aminadabu akamzaa Nashoni; Nashoni akamzaa Salmoni; Salmoni akamzaa Boazi kwa Rahabu; Boazi akamzaa Obedi kwa Ruthu; Obedi akamzaa Yese; Yese akamzaa mfalme Daudi.
Daudi akamzaa Sulemani kwa yule mke wa Uria; Sulemani akamzaa Rehoboamu; Rehoboamu akamzaa Abiya; Abiya akamzaa Asa; Asa akamzaa Yehoshafati; Yehoshafati akamzaa Yoramu; Yoramu akamzaa Uzia; Uzia akamzaa Yothamu; Yothamu akamzaa Ahazi; Ahazi akamzaa Hezekia; Hezekia akamzaa Manase; Manase akamaza Amoni; Amoni akamzaa Yosia; Yosia akamzaa Yekonia na ndugu zake, wakati wa ule uhamisho wa Babeli.
Na baada ya ule uhamisho wa Babeli, Yekonia akamzaa Shealtieli; Shealtieli akamzaa Zerubabeli; Zerubabeli akamzaa Abihudi; Abihudi akamzaa Eliakimu; Eliakimu akamzaa Azori; Azori akamzaa Sadoki; Sadoki akamzaa Akimu; Akimu akamzaa Eliudi; Eliudi akamzaa Eleazari; eleazari akamzaa Matani; Matani akamzaa Yakobo.
Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa Yesu aitwaye Kristo.
Basi vizazi vyote tangu Ibrahimu hata Daudi ni vizazi kumi na vinne; na tangu Daudi hata ule uhamisho wa Babeli ni vizazi kumi na vinne; na tangu ule uhamisho wa Babeli hata Kristo ni vizazi kumi na vinne.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Bwana.

“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumanne, Desemba 17, 2019,
Juma la 3 la Majilio

Mwa 49: 2, 8-10;
Zab 71: 1-4, 7-8, 17;
Mt 1: 1-17

JE, UNATAMBUA MPANGO WA MUNGU JUU YAKO?

Leo, tunaingia kwenye ‘oktava’ ya kujiandaa kwa karibu kabisa kwa ujio wa Kristo. Kwa siku hii, tunasikia historia ya ukoo wa Yesu. Matayo anatueleza katika mtiririko wa hali tatu ya vizazi kumi na nne. Anaanza na Abrahamu na kumalizia na Yesu. Injii inaanza kwa kumwita Yesu kuwa ni Mwana wa Daudi, Mwana wa Abraham. Hii inaonyesha muunganiko kutoka tangu ahadi za Mungu kwa Abraham, mpaka utimilifu wake katika nafsi ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.

Katika kutimiza ahadi hii, tunaona kwamba Mungu ni mwaminifu. Inachukua karne na karne, ili ahadi yake kwa Abraham itimie, lakini kwa hakika ilitimia. Hili linatueleza wazi kwamba muda wa Mungu na mpango wake juu yetu anajua muda wake wakutimiza ahadi zake, tofauti na jinsi tunavyoweza kufikiri. Tunaweza kuja na mawazo mazuri tukidhani kwamba yatapita. Lakini mara yasipopita mara moja kwa jinsi tunavyodhani na kutumaini, tunaanza kukata tamaa.

Tutafakari juu ya mipango alionayo Mungu juu ya maisha yetu. Inaweza isiwe kama tunavyodhani na kutabiri au kadiri ya jinsi tunavyoomba katika sala. Lakini inaridhisha kwamba ni kwa ajili ya uzuri wetu, ni kwasababu ya muunganiko wetu naye Mbinguni. Yesu alizaliwa ili atuvute karibu zaidi nae. Leo Yesu anatutaka mimi na wewe tuweke mipango yetu kwake na mitazamo yetu kwake. Anahitaji haya na mengine mengi. Anataka tujikabidhi sisi wenyewe kwenye mpango wake mkamilifu ndani ya moyo wa Baba yetu wa Mbinguni.

Sala: Bwana, natambua kwamba njia zako ni kamilifu na kwamba mipango yako ni mikamilifu sio yangu. Nisaidie niachane na tamaa zangu na nijikabidhi zaidi kwako, na kukuamini kabisa, na kwa yote uliopanga kwa ajili yangu. Bwana, hekima yako ni kamilifu. Nisaidie niweze kuamini hilo kwa moyo wangu wote. Yesu nakuamini wewe. Amina