ASALI MUBASHARA-Jumanne 17/12/2019

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo katika zaburi yetu ya wimbo wa katikati tunakutana na zaburi yenye kutabiri utawala wa Masiha. Utawala huu unaelezewa kama utawala wa kutamaniwa na wanaitamani ile haki itakayopatikana ndani yake.

Maskini na wanaoonewa wanategemewa kufurahia zaidi. Katika viongozi wote wa Israeli, hakuna mahali popote ambapo palitokea utimilifu wa utawala huu. Ni Masiha tu ndiye tumtegemeaye afanye ukamilifu wa utawala huu.

Somo la injili linamuonesha Masiha, yaani Yesu Kristo alitoka katika uzao wa Abrahamu. Sisi wakristo ni wazao wapya wa Abrahamu. Tulipatiwa hadhi hii kuu na Yesu. Hivyo tutambue hadhi yetu. Tujaribu kuuiga utawala wa Yesu. Kama utawala huu ulivyotamaniwa kwa hamu, sisi tuishi tunu za utawala huu hasa wale tulio viongozi.

Tuwahudumie vizuri wale tunaowaongoza, wajisikie nyumbani, wakituambia shida zao tuwajibu, tuwatie moyo, tusiwajibu kwa kashfa. Kwenye kutoa hukumu tuhakikishe tunabakia upande wa haki, tusijiunge na wenye fedha kukandamiza wanyonge au kuwatelekeza. Wao wapewe nafasi ya pekee kabisa.

Katika somo la kwanza, inadhihirishwa kwamba kabila la Yuda ambalo ndilo lililomtoa Masiha lilipatiwa baraka maalum na Baba yao yaani Yakobo. Sisi tutambue kwamba tabia njema na baraka tuzipokeazo duniani ni za muhimu sana.

Hizi zitabariki hata uzao wetu kwa siku zijazo. Tujitahidi pia kuwa na tabia njema na kujitunza katika tabia hizi njema. Wengi wetu tunapoteza mengi kwa sababu ya kutojitunza, mama Maria aliweza kuubariki ulimwengu kwa sababu ya kujitunza. Sisi tusiache kujitunza naye Bwana atatubariki. Tusiwe watu wa kukusanya laana toka kwa wenzetu tunaoishi nao hapa duniani. Tuwahudumie wenzetu nasi tutajikusanyia baraka.

Pia katika historia ya kuzaliwa kwake Yesu, kumetokea mchanganyo wa watu, wengine wameingia kibahatibahati lakini basi wanakuwa wa muhimu kwenye uzao wa Kristo. Ndivyo Mungu alivyo, ana mpango na kila mtu, hakuna aliyezaliwa, hata kama ni mwizi bado anayo nafasi mbele ya Mungu, hata kama ni mzinzi bado anayo nafasi. Mzinzi anaweza kumzaa mtoto akawa mtakatifu. Lakini mzinzi mwenyewe akaangamia. Hivyo basi tunayo hadhi kubwa mbele ya Mungu na twaweza kuwa watakatifu. Tumkimbilie na kumheshimu Mungu wetu kila wakati. Tumsifu Yesu Kristo.

©Pd. Prosper Kessy OFMCap.