ASALI MUBASHARA-Ijumaa 06/12/2019

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la injili, Bwana Yesu anawapatia vipofu uonaji. Hakika kukaa katika upofu ni jambo gumu sana. Ni vigumu kujua ukweli wa mambo yanayoendelea. Mengi tutaishiwa kudanganywa na wenzetu tu. Unapopata mwanga, ndipo unaweza kuona kivyako na kuelewa maana halisi ya vitu.

Shetani ndiye mwenye kutufanya vipofu. Mara nyingi hubovusha macho yetu, na kutufanya tushindwe kuona faida iliyopo kwenye upande wa Mungu. Yeye atatuonesha na kutufanya tuonje utamu uliopo katika ulevi, uasherati, na uvivu. Atatuzuia tushindwe kuona utamu uliopo katika kusali, katika kuwasaidia wenzetu, na kuwajali maskini. Sisi tuombe siku zote Mungu atupatie Mwanga. Atuondolee upofu wetu. Atufanye tufungue macho yetu tupate kuona faida iliyopo katika kukubali kukaripiwa, na kuishi hata na wale marafiki ambao tunadhania kwamba wanaingilia sana maisha yetu lakini kwa upande mwingine wanatupatia faida kwani hutulinda kwa maisha na mifano yao bora.

Katika somo la kwanza, linatoa habari juu ya ujio wa siku; siku ya matumaini kwa wanyenyekevu na walio katika giza. Siku hiyo inatangazwa kuwa nzuri kwa Lebanoni, inatangazwa kuwa nzuri kwa vipofu, na viziwi. Mwenye kuonea wengine ataangamizwa, na mwenye dharau atakoma kabisa. Wengi watapata kumfahamu Mwenyezi Mungu.

Hakika hii ni siku ya furaha, na Yesu mwenyewe ndiye atakayeikamilisha. Wanadamu huwa hatudumu kwenye nguvu zetu, au cheo chetu au afya yetu hadi mwisho.

Sisi ipo siku sisi tulio na majivuno tutakoma. Yesu ndiye mwenye kubaki milele. Alipokuja kwa mara ya kwanza alituonjesha kile atakachokamilisha ajapo kwa mara ya pili. Hivyo tujifunze kuwa na tabia za kinyenyekevu, tujue kwamba tunaisubiri siku nzuri, siku ya furaha. Hata na wale tunaoumwa, hakika tujue kwamba siku ya namna hiyo itakuja kwetu. Ipo siku Bwana ataondoa na kufuta machozi yote.

©Pd. Prosper Kessy OFMCap.