ASALI MUBASHARA-Alhamisi 05/12/2019

Karibuni sana wapendwa wangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo Bwana Yesu anatolea mfano toka katika mazingira yenye mafuriko makali. Mazingira haya kwa wakati wa kiangazi huonekana kuwa salama, yenye kuvutia na yenye majani mazuri. Atakayejenga nyumba yake bila kuchunguza vyema juu ya ugumu wa eneo hilo, bila kuuliza namna jinsi hali ilivyo kwa kipindi cha mafuriko na dhoruba, hakika huyo ataishia kupoteza nyumba yake na mali zake.

Lakini anayeulizia hali ya majira ya mafuriko kabla ya kujenga hakika huyo ingawa atachukua muda kabla ya kujenga, ataweza kujipanga vizuri na kujenga vitu imara na hivyo kutumia mali yake vyema. Yesu anataka kutuambia kwamba tunapoalikwa kumfuata yeye, tuingia kama askari imara. Tusitegemee kwamba hali itakuwa shwari siku zote kila tunapomfuata Yesu. Upo wakati maadui watashambulia na ikiwa tupo imara, ndipo tutakapoweza kusalimika. Tukiwa watu wa kuita Bwana Bwana kwa midomo yetu tu bila kuonesha uwajibikaji, kwa hakika tutashindwa na kila kishawishi kitakachotokea.

Tuwe watu wa kuijenga imani yetu kwa sala na maandiko matakatifu. Tuwe watu wa kutubu kila wakati, hata ikiwa tunarudia kuungama dhambi zile zile, lakini tusichoke kutubu kwa kila wakati. Pale tunapojiona kuridhika sana na kuacha kusali ndipo shetani hushambulia na kuharibu zaidi. Siku zote tujione kuwa wahitaji.

Katika somo la kwanza, Nabii Isaya anatoa unabii wa wimbo wenye kueleza juu ya nyakati zijazo, kwamba mji wa Yuda utakuwa na nguvu, kwani Mungu atakuwa katikati yake. Na taifa litakaloingia ndani yake ni lile lishikalo haki na kweli na lenye kumtegemea Mwenyezi Mungu. Lakini ile miji iliyojiona ipo juu, na yenye nguvu, hakika hiyo itashushwa kwa sababu haina Bwana ndani yake.

Sisi tutambue kwamba ikiwa hatuna Bwana ndani yetu, ikiwa tupo wakavu kiimani, hakika hatutakuwa na chochote chenye kutushikilia ili tusipate kuanguka. Kristo ndiye mwenye kutubeba na kutuweka juu. Tusichoke kumwelekea ili atupatie ushindi. Tumsifu Yesu Kristo.

©Pd. Prosper Kessy OFMCap.