Pope Francis celebrates a Mass at the National Stadium, Thursday, Nov. 21, 2019, in Bangkok, Thailand. (AP Photo/Gregorio Borgia)
SOMO 1. Danieli 6:12-28…Ndipo wakakaribia, wakasema mbele ya mfalme katika habari ya ile marufuku ya mfalme; Je! Hukuitia sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba? Mfalme akajibu, akasema, Neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza kubadilika.
Basi wakajibu, wakasema mbele ya mfalme, Yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku.
Basi mfalme aliposikia maneno haya alikasirika sana, akakaza moyo wake ili kumponya Danieli; akajitaabisha kumwokoa hata jua likachwa.
Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia mfalme, Ee mfalme, ujue ya kuwa ni sheria ya Wamedi na Waajemi, lisibadilike neno lo lote lililo marufuku, wala amri yo yote iliyowekwa na mfalme.
Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya.
Likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu; naye mfalme akalitia muhuri kwa muhuri yake mwenyewe, na kwa muhuri ya wakuu wake, lisibadilike neno lo lote katika habari za Danieli.
Kisha mfalme akaenda nyumbani kwake, akakesha usiku kucha, akafunga; na vinanda havikuletwa mbele yake; na usingizi wake ukampaa.
Asubuhi mfalme akaondoka mapema, akaenda kwa haraka mpaka penye lile tundu la simba.
Naye alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danieli, Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa?
Ndipo Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele.
Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno.
Basi mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danieli katika lile tundu. Ndipo Danieli akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake, kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake.
Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danieli, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu.
Ndipo mfalme Dario akawaandikia watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, waliokaa juu ya uso wa dunia; Amani na iongezeke kwenu.
Mimi naweka amri, ya kwamba katika mamlaka yote ya ufalme wangu watu watetemeke na kuogopa mbele za Mungu wa Danieli; maana yeye ndiye Mungu aliye hai, adumuye milele, na ufalme wake ni ufalme usioharibika, na mamlaka yake itadumu hata mwisho.
Yeye huponya na kuokoa, hutenda ishara na maajabu mbinguni na duniani, ndiye aliyemponya Danieli na nguvu za simba.
Basi Danieli huyo akafanikiwa katika enzi ya Dario, na katika enzi ya Koreshi, Mwajemi.Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 100 (K) Ufu. 19:9

(K) Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwanakondoo.

Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote,
Mtumikieni Bwana kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba. (K)

Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (K)

Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru;
Nyuani mwake kwa kusifu;
Mshukuruni, lihimidini jina lake. (K)

Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)

SHANGILIO
Zab. 25:4 , 5

Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, unijulishe njia zako, unifundishe mapito yako.
Aleluya.

INJILI
Lk. 21:20-28

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia. Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie. Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapitilizo, ili yatimizwe yote

yaliyoandikwa. Ole wao wenye miamba na wanaonyonyesha katika siku hizo!
Kwa kuwa kutakuwa na shida katika nchi, na hasira juu ya taifa hili. Wataanguka kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara na kuchukuliwa katika mataifa yote; na Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa, hata majira ya Mataifa yatakapotimia.
Tena, kutakuwa na ishara katika jua; na mwenye, na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake; watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazama mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu z ambinguni zitatikisika. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi. Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.

*ASALI MUBASHARA-Alhamisi 28/11/2019*

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo katika somo la kwanza tunapata habari juu ya imani ya Daniel. Aliweza kuwa na imani kati kati ya wageni, wageni waliokuwa na roho mbaya juu yake, waliotaka aikane imani yake. Hivyo walimzunguka kila upande kwa sababu ya imani yake.

Leo tunasikia wakimshtaki kwa mfalme ili uhai wake uondolewe. Lakini Mwenyezi Mungu anakuwa upande wake. Daniel anamlimlia Mungu na kwa hakika anapata kuokolewa. Matendo ya kufanyiwa fitina kama alivyofanyiwa Danieli wanafanyiwa wengi kwa nyakati zetu.

 

Wapo kati yetu wenye umbea, wenye kufuatilia mambo ya watu, tusiotaka watu waishi bila uhuru, wafuatiliwe kila wanapokanyaga-kila wanachotenda kinaripotiwa-hakika hizi sio tabia za kimungu. Wanadamu wanapaswa kuishi katika uhuru, hata kama ni mke au mume anapaswa apewe uhuru na si kuishi kitumwa akifuatiliwa kama mhalifu. Hivyo tuwe watu wa kuwapenda wenzetu waishi kiuhuru, tusiwabane sana watu, tusiwe watu wa kutazama au kufuatilia kila kitu chao. Tabia za namna hii zinatufanya tutende dhambi kila siku.

 

Binadamu ni tofauti na simu yako au miguu yako ambayo kila wakati unapaswa kuitazama. Wanadamu wameumbwa ili waishi kwa uhuru. Tukiwa na tabia za kufuatilia kila ya mwenzetu hakika tutaishia kuwafitini na kuwaumiza wenzetu kila siku.

 

Katika somo la injili, Yesu anaelezea juu ya ujio wa nyakati ngumu kwa mji wa Yerusalem. Yerusalemu uliaminiwa kuwa mji wa amani lakini habari zinazoelezwa juu yake leo kwa hakika ni tofauti, sio habari za amani. Yerusalemu ilishindwa kupalilia amani yake kwa njia ya sala na kufanya toba na matendo mema. Mwishowe amani yao inachezewa na wao kuishi katika huzuni. Nasi tujitahidi kutambua kwamba tunaweza kuichezea amani yetu na kuishia kwenye magumu kama yaliyotokea kwa Yerusalemu, mji uliotangazwa kuwa mji wa amani.

 

Hivyo tusiwe watu wa kuendeleza siasa za chuki, za ukabila, unyanyasaji. Hizi zitatufanya tuikose imani kwa hakika. Tujitahidi kukuza amani. Tumsifu Yesu Kristo.

Copyright:Pd. Prosper Kessy OFMCap.

NB:
*Jipatie Shajara ya ASALI MUBASHARA 2020. Kama unahitaji wasiliana nami sasa zipo za kutosha 0714002466 au 0755444471. Jipatie Shajara hii tuinjilishe Ulimwengu watu wamjue Mungu.*