MASOMO YA MISA NOVEMBA 25, 2019
JUMATATU, JUMA LA 34 LA MWAKA

SOMO 1
Dan. 1:1-6,8-20

Katika mwaka wa tatu wa kumiliki kwake Yehohakimu, mfalme wa Yuda, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alikwenda Yerusalemu akauhusuru. Bwana akamtia Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika mkono wake, pamoja na baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mungu; naye akavichukua mpaka nchi ya Shinari, mpaka nyumba ya mungu wake; akaviingiza vile vyombo katika nyumba ya hazina ya mungu wake.
Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu wa matoashi wake, awalete baadhi ya wana wa Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa uzao wa kiungwana; vijana wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu; tena alimwambia awafundishe elimu ya Wakaldayo, na lugha yao. Huyo mfalme akawaagizia posho ya chakula cha mfalme, na ya divai aliyokunywa, akaagiza walishwe hivyo muda wa miaka mitatu; ili kwamba hatimaye wasimame mbele ya mfalme.
Basi katika hao walikuwapo baadhi ya wana wa Yuda, Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria. Lakini Danieli aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa; basi akamomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa asijitie unajisi. Basi Mungu alimjalia Danieli kupata kibali na huruma machoni pa huyo mkuu wa matowashi. Mkuu wa matowashi akamwambia Danieli, Mimi namwogopa bwana wangu, mfalme, aliyewaagizia ninyi chakula chenu na kinywaji chenu; kwa nini azione nyuso zenu kuwa hazipendezi kama nyuso za vijana hirimu zenu? Basi kwa kufanya hivyo mtahatirisha kichwa change mbele ya mfalme.
Ndipo Danieli akamwambia yule msimamizi, ambaye mkuu wa matowashi amemweka juu ya Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria, Tafadhali utujaribu sisi watumishi wako muda wa siku kumi; na watupe mtama tule, na maji tunywe. Kisha nyso zetu zitazamwe mbele yako, na nyuso za wale vijana wanaokula chakula cha mfalme; ukatutendee sisi watumishi wako kadiri ya utakavyoona. Basi akawasikiliza katika jambo hilo, akawajaribu siku kumi. Hata mwisho wa zile siku kumi nyuso zao zilikuwa nzuri zaidi, na miili yao ilikuwa imenenepa zaidi, kuliko wale vijana wote waliokula chakula cha mfalme. Basi yule msimamizai akaiondoa posho yao ya chakula, na ile divai waliyopewa wanywe, akawapa mtama tu.
Basi, kwa habari za hao vijana wanne, Mungu aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danieli naye alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto. Hata mwisho wa siku zile alizoagiza mfalme za kuwaingiza, mkuu wa matowashi akawaingiza mbele ya mfalme Nebukadreza. Naye mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote hawakuonekana waliokuwa kama Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria; kwa hiyo wakasimama mbele ya mfalme. Na katika kila jambo la hekima na ufahamu aliowauliza mfalme, akawaona kuwa walifaa mara kumi zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Dan. 3:52-56 (K)

(K) Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Umehimidiwa, Ee Bwana, Mungu wa baba zetu,
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
Limehimidiwa jina lako takatifu, tukufu;
Lastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele. (K)

Umehimidiwa katika hekalu la fahari yako takatifu,
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. (K)

Umehimidiwa utazamaye vilindi,
Uketiye juu ya makerubi;
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele. (K)

Umehimidiwa katika anga la mbinguni,
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. (K)

SHANGILIO
2Tim. 1:10

Aleluya, aleluya,
Mwokozi wetu Yesu Kristu alibatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika kwa Injili.
Aleluya.

INJILI
Lk. 21:1-4

Yesu aliinua macho yake akawaona matajiri wakiitia sadaka zao katika sanduku la hazina. Akamwona mjane mmoja maskini akitia mle senti mbili. Akasema, Hakika nawaambieni, huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote; maana, hao wote walitia sadakani katika mali iliyowazidi, bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.