MASOMO YA MISA JUMAPILI NOV 24 2019.
DOMINIKA YA KRISTO MFALME MWAKA C
SOMO 1
2 Sam 5: 1-3
Somo katika kitabu cha pili cha Nabii Samweli
Ndipo kabila zote za Israeli wakamwendea Daudi huko Hebroni, wakasema naye, wakinena, Tazama sisi tu mfupa wako na nyama yako. Zamani za kale, hapo Sauli alipokuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyewaongoza Israeli watoke nje, na kuingia ndani. Naye Bwana akakuambia, wewe utawalisha watu wangu Israeli, nawe utakuwa mkuu juu ya Israeli. Basi, wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni; naye mfalme Daudi akapatana nao huko Hebroni mbele za Bwana; wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya Israeli.
Neno La Bwana……….Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI:
Zab 122:1-5
(K)Nalifurahi waliponiambia, na twende nyumbani kwa Bwana.
Nalifurahi waliponiambia,
na twende nyumbani mwa Bwana.
Miguu yetu imesimama,
ndani ya malango yako ee Yerusalemu. (R)
Ee Yerusalemu uliyejengwa,
kama mji ulioshikamana;
huko ndiko waliko-panda kabila,
kabila za Bwana. (R)
Ushuhuda kwa Israeli,
walishukuru jina la Bwana.
Maana huko viliwekwa viti vya hukumu,
viti vya enzi vya nyumba ya Daudi. (R)
SOMO LA PILI:
Kol. 1:11-20
Somo katika waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai.
Mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha; mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;
ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi. Naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivya juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana, ikiwa ni viti vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake, akiisha kufanya Amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.
Neno La Bwana…………Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO.
Mariko 11:9b, 10a
Aleluya, Aleluya,
Abarikiwe Yeye ajaye kwa jina la Bwana, Ubarikiwe na ufalme ujao, wa baba yetu Daudi.
Aleluya
INJILI:
Luka. 23: 35-43
Watu walisimama wakimtazama Yesu. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake. Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki, huku wakisema, kama wewe ndiwe mfalme wa wayahudi, ujiokoe mwenyewe. Na juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI. Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi. Lakini yule wa pili akamjibu, akamkemea akisema, wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tulivyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa. Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi.
Neno la Bwana……Sifa kwako ee kristo.