Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. –Neno la Bwana katika somo la kwanza, tunasikia habari za Mfalme Antiokus na kuingia kwa upagani katika Israeli ambapo Yuda analazimishwa kuziacha tamaduni zake zilizomfikisha hapo alipo na kukumbatia tamaduni nyingine za kigeni.
Siku ya leo anatokea Mfalme Antiokus analazimisha kwamba watu waache kumwabudu Bwana Mungu wa Israeli, waache tamaduni zao, na vitabu vya sheria, yaani Biblia takatifu ichanwe halafu zifuatwe tamaduni za taifa jingine. Kwa Israeli, kama inavyooneshwa katika Kumbukumbu la Torati 6:4, tamaduni zao na sheria zilikuwa takatifu na waliambiwa kwamba ndio zitakazowalinda kama taifa. Hivyo walielezwa kwamba wasizitupe, bali wawafundishe na vizazi vijavyo.
Sasa leo Antiokus anawaeleza kwamba wasizifuate. Na mbaya zaidi wapo baadhi ya Wayahudi waliotaka kuzitupa tamaduni zao. Lakini wengi kati ya Israeli watanyanyuka na kupambana na uonevu huu.
Somo hili litoe kwetu pia hamasa kuzitetea tamaduni zetu kama wakristo. Siku hizi tumevamiwa na kundi la utamaduni wa ukisasa unaoona kama tamaduni zetu kama kanisa zimekwishapitwa na wakati. Hivyo wanataka nyingine zijitokeze juu yao. Sisi tuwe tayari kupambana na uonevu wa namna hii. Hatuwezi kuutupa utamaduni wetu pembeni kwani huu ndio uliotufikisha hapa tulipo.
Pia hatupaswi kutupa baadhi ya tamaduni na desturi zetu za makabila ya asili kwani nazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kutufikisha hapa tulipo. Ukweli ni kwamba vipo baadhi ya vitu ndani ya tamaduni za makabila yetu ya asili vinavyopaswa kuboreshwa lakini hatupaswi kutupa desturi na tamaduni zetu zote. Mara nyingi waliolelewa kufuatana na mila na desturi za kabila lao wanakuwa wafanisi, wenye heshima kwa wazee, hofu ya Mungu na sio wabinafsi kwani tamaduni za makabila mengi hupinga ubinafsi. Waliokosa malezi toka kwa makabila yao mara nyingi huwa wabinafsi. Hivyo tujifunze kuheshimu tamaduni zetu.
Katika somo la injili, kipofu wa Yeriko anapata uponyaji. Kipofu huyu kwa hakika alianza kwa kunyamazishwa na waliokuwa pembeni lakini yeye akagundua kwamba wao sio watu wema. Hivyo aliamua kujitosa mwenyewe na kumwita Yesu. Na kwa hakika alitumia muda ule vizuri kwani hii ilikuwa ni mara ya mwisho ya Yesu kuja Yeriko. Hivyo alitumia muda huu kama “golden chance”.
Nasi tujifunze kutumia fursa zetu vizuri. Upo wakati ambao fursa nyingi zitajitokeza lakini haitakuwa hivyo kwa kipindi chote. Tujifunze kutumia chance vyema. Kila fursa inayojitokeza kwa hakika itumiwe, isitupwe pembeni.
©Pd. Prosper Kessy OFMCap.
*NB: Ukihitaji shajara ya “ASALI MUBASHARA” ya mwaka 2020 yenye masomo ya kila siku na tafakari zake za Asali Mubashara mwaka mzima wasiliana nami kwa number hizi 0755444471 au 0714002466. Shajara imeshiba na masomo mpaka na zaburi zimechambuliwa kuongeza ufahamu wa maandiko na kukuza hekima yetu kwa Mungu.* *Ukiipata utaipenda mwenyewe, itakusaidia mnoo*