Mwezi wa 10 ni mwezi rasmi wa Umisionari. Kariba misa ya shukrani ya birthday ya baba yetu Kardinal Pengo, aliwakabidhi madekano misalaba kuipeleka katika maparokia na ikiwezekana misalaba ifikie jumuia na hata familia zetu.
Baba mtoa mada alisisitiza kuwa Umisionari tuliouchagua sio kitu kidogo. Umisionari ni utendaji na kujituma.
Umisionari lazima utoke moyoni yaani ni kitu kilicho ndani kabisa.
Umisionari sio tu kupeleka vitu kwa wahitaji kwani hata mashetani wanapeleka vitu. Umisionari ni lazima pia kupeleka habari njema kwa watu walio na uhitaji.
Jambo la muhimu kabisa kujitambua sisi ni kina nani.
Kila mbatizwa anapaswa kuwa na roho ya kimisionari. Kila mbatizwa anapatakiwa kuwa na utayari wa kumtangaza Yesu Kristu bila woga, wala wasiwasi ama kujionea huruma na bila kujali changamoto yoyote.
Wamisionari wa kwanza hawakuona kuwa maisha yao ni kitu na ndio maana walikuwa tayari kutumwa.
Roho ya Umisionari inapaswa ikue, ichipue, istawi ndani ya mioyo yetu ni kisha itoke nje kufaidisha wengine.
Umisionari ni upendo na huanza kwenye familia.
Kwa asili katika ubatizo tunadhiriki ofisi zifuatazo tatu na Bwana wetu Yesu Kristu: Ukuhani, Unabii na Ufalme
Lakini hatuwezi kuongelea roho ya kimisionari bila kuzungumzia utume (yaani kutumwa na kujituma)
Mmisionari ni mtume. Sio mtu anayejifungia ndani bali anayetoka na kuwaendea wengine. Kwahiyo sio rahisi kufanya kazi ya Kimisionari bila kufanya utume.
Kazi tunayofanya sisi ni Utume hivyo inapaswa kuendana na maisha yetu ya kila siku. Ujumbe tunaovaa unainjilisha hivyo ni muhimu utume uonekane katika jamii na mazingira yetu ya kawaida.
Rejea maandiko yafuatayo: Mathayo 10:5-7, Marko 6:7, 10-12 na Luka 9:1-2; 10:1 ambayo yote yanatuusia juu ya kutumwa.
Utume ni kupeleka habari njema ya kimisionari. Rejea Marko 16:15-16
Fr Msafiri alisisitiza kuwa tunaweza fanya zaidi ya mapadre kwakuwa tunawafuata watu katika mazingira tofauti. Ni hii ni katika kuboresha zaidi utume wetu.
Watu wanajifunza naa kufuata maisha tuishiyo na kuiga tufanyayo. Hivyo basi matoleo yetu ya kimwili yaendane na ya kiroho.
Mmsionari anapaswa atumie karama zake alizopewa na Mungu kwa ajili ya kuwanufaisha wengine na kufaidiana. Rejea 1Tim 4:14
* Kila mbatizwa ana karama.
Karama tulizopewa sio za kujifaidisha wenyewe bali wote watuzungukao na wenye uhitaji. Hivyo basi kwa lugha nyingine tunapaswa kuwa sauti ya wanyonge
Mmisionari ni mtu anayepeleka habari njema kwa watu mahali ambapo haijafika na hivyo basi tunapaswa kwenda kuwagusa wahitaji wainuke pale walipo.
Baba alitupa mfano wa Sudan. Kuna parokia kadhaa zinafungwa na mapadre hawana pa kwenda. Lakini pia hata wakihitaji kwenda kwenye mafungo hakuna wa kuwategemeza. Tunapaswa kuangalia wahitaji wa namna hii.
Pia tulipatiwa mfano wa Tabora. Kuna kituo kina watu walioumbwa kwa jinsi ya ajabu kabisa. Mtu kazaliwa na mguu mmoja na mwingine jicho kwenye utosi. Yafaa kufika maeneo kama haya pia. Yatatusaidia pia kutafakari ukuu wa Mungu.
Ila kuna watu wanahitaji kusikia habari njema sio kwasababu hawajasikia bali wanahitaji kusikia upya wapate kuamka.
Sio lazima mtu kuwa na utume maalumu bali haya yote twaweza fanya katika kazi zetu, matendo yetu, kutembelea na kusaidia wahitaji. Pia kufanya injili ya upendo. Kuna watu wanasikia na kuhubiriwa juu ya upendo ila hawajawahi kuuonja upendo huo.
Wapo pia wanaofikiri wanajua kila kitu nao wanahitaji kufikiwa.
Mmsionari ni mtu anayetoa maelekezo, anayeonyesha na anayefundisha. Hivyo basi tutoe vitu kwa wahitaji lakini pia tufundishe Injili. Wenzeti wanasema ‘Materials perish but knowledge never perishes’ yaani ‘Vitu vinaisha lakini ujuzi kamwe hauwezi isha/kupotea’.
Pia tumesisitizwa kuitumia mitandao vyema na kweli kwa ajili ya Umisionari. Tunatakiwa kuwafundisha watu athari za mitandao ya kijamii na kupiga vita matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii. Tunapaswa kuwa wa kwanza kufindisha, kuonya na kuelekeza.
Tunatakiwa zaidi kufundisha watoto juu ya haya yote. Siku hizi watoto wadogo wanatumia mitandao ya kijamii kufanya mambo ya ajabu. Sisi tuna nafasi kubwa sana ya kufundisha juu ya hili.
Hapa baba alitueleza jambo. Aliwahi kukusanya watoto kati ya umri wa miaka 7-13 na kufanya semina nao. Aliwaambia waandike kwenye vikaratasi vitu gani wamejifinza katika mitandao. Kuna mmoja akasema yeye alikuwa wa kwanza darani akapewa zawadi ya simu na mama yake ili aweze jisomea zaidi kwenye mitandao. Lakini matoke yake amekuwa mtu wa kuangalia picha mbaya na hata darasani ameshuka sana hivyo mitandao imemuharibu.
Je! Umisionari wetu unatusaidia nini kama kuanzia katika familia zetu mitandao imetuathiri?
Halikadhalika, mmsionari ni yule anayejituma mwenyewe. Umisionari sio tendo la kutimiza wajibu bali tendo la upendo linalotakiwa kuchipuka toka moyoni.
Tunafundishwa kuwa hata wamisionari wa kwanza walijituma. Rejea Isaya 6:8-10
Nasi tumeitika kwa kuwa tayari wakati wowote.
Mungu aliona jinsi mitandao itakavyoharibu ulimwengu na akatuchagua nasi tukaitika na kujitoa kwa moyo mmoja. Basi yafaa tuanze kufanya mambo pasipo kusukumwa.
Tunabeba ujumbe mzito katika tshirt zetu ‘Mimi hapa nitume Bwana’. Hatuwezi kujivunia Ukatoliki wetu ilhali hatutaki kujituma.
Tukifanya kazi kwa moyo, amani na utulivu tutafurahia utume na kuufanya priority kwetu. Tukumbuke jinsi Ibrahim alivyojitoa na akakubali kwa moyo mweupe kutumwa pamoja na uzee wake.
Mara nyingi tunakuwa tayari kujituma kwa ajili ya mambo ya ulimwengu sio kwa ajili ya Injili.
Mtume Paulo alisema ‘Ole wangu mimi nisipoihubiri Injili.’ Nasi Ole tuna ole tusipotimiza wajibu.
Je! Utume wangu una nafasi gani katika maisha yangu? Tunapaswa kujitoa kama zawadi kwa ajili ya watu wengine.
Yesu Kristu ni Mmisionari namba moja aliyekubali kuacha Umungu wake akawa binadamu tangu kuzaliwa (ila tu hakuwa na dhambi). Pia alichagua kuzaliwa katika familia maskini. Pia akawa katika hali ya mkate apate kutulisha na kuinjilisha iwe rahisi kumpokea.
Kujituma mwenyewe kuna faida kubwa sana mbele ya Mungu kuliko kutumwa/kusukumwa.
Kazi ifanyikayo kwa kusukumwa hufanywa kwa woga na huwa chini ya kiwango. Kufanya kazi kwa kujituma husababisha mtu kufanya kazi kwa amani na furaha na matokeo yake ni makubwa.
Fr Msafiri anaendelea kusisitiza kuwa ni Utume wa pekee tulionao na yatupasa kufikiri tena na tena jinsi tunavyoufanya.
Inatupasa kujitambua na kila mara kujiuliza , ‘Mimi ni nani? Ninaufanyia kazi Umisionari wangu? Ninaitikia wito wangu sawa sawa?’
Mwisho kabisa anatuombea baraka na neema. Daima uso wa Mungu uwe pamoja nasi. Tuitikie Utume ili uzae matunda mema huko mbinguni!!!!
Tumsifu Yesu Kristu!